Ungana nasi kwa kuandika email yako hapa ili upate habari mpya kupitia email yako bila usumbufu:


Home » » MKURUGENZI WA UPELELEZI WA MAKOSA YA JINAI ( DCI) , ROBERT MANUMBA NI MAHUTUTI NA AMELAZWA AGA KHAN

MKURUGENZI WA UPELELEZI WA MAKOSA YA JINAI ( DCI) , ROBERT MANUMBA NI MAHUTUTI NA AMELAZWA AGA KHAN

tangazo

HALI ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Jeshi la Polisi (DCI), Kamishna Robert Manumba ni mbaya na amelazwa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU), Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.Habari zilizopatikana jana zilieleza kuwa Manumba amelazwa hospitalini hapo baada ya kusumbuliwa na maradhi kadhaa, ikiwamo figo.



Taarifa za ndani kutoka Jeshi la Polisi zilisema jana kuwa tangu juzi, Manumba alikuwa hajitambui baada ya kuugua malaria ghafla na hali hiyo ilisababisha pia figo zake zote mbili kushindwa kufanya kazi.

“Alitakiwa kupelekwa nje ya nchi kwa matibabu, lakini ilishindikana kwa sababu hajitambui, wakajaribu kumzindua, ikashindikana,” kilieleza chanzo hicho cha habari ndani ya jeshi hilo.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso, alithibitisha kamishna huyo kulazwa ICU Aga Khan lakini akasema kuwa hadi jana jioni, hali yake ilikuwa ikiendelea vizuri.

“Ni kweli amelazwa katika hospitali ya Aga Khan, lakini hali yake inaendelea vizuri,” alisema Senso.

Mtu wa karibu na Manumba, alisema, Manumba alikutwa na vijidudu 500 vya malaria, tatizo ambalo lilisababisha pia viungo vyake vingi, ikiwamo figo kushindwa kufanya kazi.

“Kutokana na hali aliyonayo tumeshindwa kumsafirisha kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu zaidi kwa sababu baadhi ya viungo havifanyi kazi,” alisema mtu huyo.

Hata hivyo, alisema hali ya Manumba inaendelea vyema baada ya kuanza kupata matibabu.

JK amjulia hali
Viongozi mbalimbali wa Serikali, akiwamo Rais Jakaya Kikwete jana walifika hospitalini hapo kumjulia hali kamishna huyo wa polisi.

Habari zilizopatikana zilieleza kuwa Rais Kikwete alifika hospitalini hapo jana mchana baada ya kumsindikiza mgeni wake, Rais wa Benin ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Boni Yayi.

Daktari
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Aga Khan, Dk Jaffer Dharsee alisema jana kwamba Manumba alifikishwa katika hospitali hiyo tangu juzi akisumbuliwa na malaria na alikuwa hajitambui.

Dk Dharsee alisema kuwa uchunguzi wa awali ulionyesha kwamba alikuwa na malaria kali iliyosababisha alazwe ICU. Hata hivyo, alisema baada ya matibabu, hali yake ilianza kubadilika na kuleta matumaini.

“Nimepigiwa simu nyingi leo (jana), nikiulizwa na watu mbalimbali wakitaka kufahamu kama Manumba amefariki dunia, ninachotaka kuwaambia ni kwamba ni mzima lakini yuko ICU,” alisema.
TUPE MAONI YAKO
KAMA UMEGUSWA NA HUDUMA ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
KUMBUKA KU LIKE UKURASA WETU WA FACEBOOK
 
Support : mpekuzi | John mpekuzi | Wataalam
Copyright © 2009. DOMO LANGU - All Rights Reserved
Template designed by mpekuzi
Proudly powered by Blogger