tangazo
MKAZI
wa kijiji cha Turiani, Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, Athuman Rashid
(25) amehukumiwa kutumikia kifungo cha maisha jela na adhabu ya kuchapwa
viboko sita baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mtoto wa miaka
saba.
Hukumu
hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Korogwe, Arnold Kirekiano.
Kwa
mujibu wa hati ya mashitaka iliyosomwa na Mwendesha Mashtaka wa Polisi,
Janson Zakaria alidai Athuman alitenda kosa hilo Juni 21 mwaka jana,
saa 11.00 jioni katika kijiji cha Turiani wilayani hapo.
Hati
hiyo ya mashitaka inadai Athuman alimuita mtoto huyo ambaye alikuwa
akiishi na bibi yake kijijini hapo kwa lengo la kumtuma dukani ndipo
alipomtendea unyama huo.
“Alipokuwa
akifanyiwa tendo hilo mtoto huyo alipiga kelele na baadhi ya majirani
kujitokeza kufika eneo hilo huku, mtoto huyo akilalamika kwa maumivu
sehemu ya siri na akimtaja mtuhumiwa,” alidai Zakaria.
Kabla
ya Hakimu Kirekiano kutoa hukumu alimtaka mshitakiwa kama ana chochote
cha kujitetea aeleze mahakamani; naye akasema hana cha kujitetea,
Mahakama iamue.
Hakimu alisema kifungo hicho cha maisha jela na viboko sita, iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.


