tangazo
SIKU chache baada ya kikundi cha Al Shabaab kudaiwa kuteka Jengo la
Westgate nchini Kenya na kuua watu kadhaa na wengine kujeruhiwa wasiwasi
wa magaidi kulipua tena nchi hiyo umetanda.
Tayari Marekani imetoa angalizo kwa Kenya kuhusu uvamizi huo na
kuitaka isibeze kuchukua tahadhari kama ilivyofanya kwa tukio la
Westgate na kusababisha madhara makubwa kwa wananchi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Baraza la Ushauri
la Usalama wa Nje la Marekani ni kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kutokea
tena kwa shambulizi la ugaidi nchini Kenya.
Marekani imesema shambulio hilo litafanywa na kundi jipya la
wanamgambo wa Kenya la Al Hijra ambalo linashirikiana na Al Shabaab na
lengo lake ni kuharibu maeneo nyeti.
Kutokana na hali hiyo, Serikali ya Marekani imewataka raia wake kuwa
makini wakati wanapokuwa kwenye maeneo ya umma katika miji ya Nairobi na
Mombasa.
Tahadhari hiyo imekuja ikiwa ni siku kadhaa baada ya Al Shabaab kuishambulia
Kenya mwaka huu na Uganda mwaka 2010 na kusababisha vifo vya watu 77 ambao walikuwa
wanaangalia mchezo wa mpira kwa njia ya televisheni.
Tukio la Westgate lilisababisha Umoja wa Mataifa (UN), Uingereza,
Marekani na mataifa mengine makubwa kuelekeza masikio nchini Kenya
kutokana na kushtushwa na shambulio hilo.
-Gazeti la Jambo leo