tangazo
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
Wizi huo ambao umewasababishia hasara kubwa baadhi ya wasafiri
wakiwamo wafanyabiashara, abiria wa kawaida na watalii wanaoingia
nchini, unadaiwa kufanywa na baadhi ya wafanyakazi wa Wakala wa Mizigo
wa Kampuni ya Swissport.
Wafanyakazi hao wamekuwa wakiiba vifaa na bidhaa kwa kuchana
mabegi ya abiria kisha kuviweka kwenye makoti yao ya kazi lakini kwa
mizigo mikubwa, wamekuwa wakiificha kwenye magari ya zimamoto ambayo
huingia na kutoka ndani ya uwanja wa ndege bila kufanyiwa ukaguzi.
Chanzo kingine cha habari katika uwanja huo kinasema magari ya
zimamoto yanayofanya kazi katika uwanja huo hayakaguliwi yanapopita
kwenye lango kuu, hivyo kutoa mwanya wa kuvushwa kwa mali za wizi.
“Mali zinazowekwa katika magari hayo ni zile kubwa ambazo
hutakiwa kuuzwa nje ya uwanja wa ndege kama kontena la simu au mabegi
makubwa ya nguo,” kilisema chanzo hicho.
Baadhi ya waathirika wa wizi huo waliliambia gazeti hili kwamba
wamepoteza mizigo mingi kwa nyakati tofauti na kupata hasara kubwa na
kwamba uwanja huo si salama kwa wafanyabiashara hasa wanaoingiza bidhaa
zao kutoka nje ya nchi.
Chanzo chetu katika uwanja huo kilidokeza kuwa mara nyingi wizi
hufanyika wakati mizigo inaposhushwa kutoka kwenye ndege kupelekwa eneo
la kusubiri kuchukuliwa na abiria pia wakati mizigo mingine
inapohifadhiwa kwenye stoo uwanjani hapo ikisubiri wahusika kuichukua.
“Wakati wanashusha mizigo kutoka kwenye ndege wanaikata kwa visu
au viwembe vikali na kuchomoa chochote kilichomo kisha wanaweka katika
makoti ya kazi ambayo yana mifuko mikubwa,” kilieleza chanzo hicho.
Mkurugenzi Mtendaji wa Swissport Tanzania, Gaudence Temu alikiri
kuwapo kwa tatizo hilo lakini akasema kampuni yake kwa kushirikiana na
wadau wengine uwanjani hapo wamekuwa wakichukua hatua za kudhibiti wizi
huo.
“Huu wizi unaharibu sifa ya uwanja wa ndege wa kimataifa, ndiyo
maana tukasema hatutakuwa na uvumilivu hata kidogo kwa wale ambao
tunabaini kwamba wanafanya vitendo hivyo,” alisema Temu.
Kamishna Msaidizi wa Zimamoto na Uokoaji, Sikiri Sala alisema
amekwishazungumza na Kikosi cha Zimamoto Uwanja wa Ndege kuhusu suala
hilo ambalo hata hivyo, alisema ni zito na linahitaji ushirikishwaji wa
viongozi wote kwa kuwa uwanja huo una mashirika mengi.Soma zaidi: mwananchi.co.tz