tangazo
Utangulizi
Ndugu wananchi;
Namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujalia uzima na kutuwezesha kuwasiliana kupitia utaratibu wetu mzuri tuliojiwekea wa kufanya hivyo kila mwisho wa
mwezi. Leo nimepanga kuzungumza nanyi mambo matatu; yaani Mpango wa
Amani, Usalama na Ushirikiano wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo,
Uhusiano wa Waislamu na Wakristo na Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha
Nne.
Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano wa
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo
Ndugu Wananchi;
Tarehe
8 Februari, 2013 kule Addis Ababa, Ethiopia niliungana na Katibu Mkuu
wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Ban Ki-Moon, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja
wa Afrika, Mhe. Nkosozana Dlamini Zuma na viongozi wa nchi 12 za Afrika
Mashariki, Kati na Kusini kutia saini Mpango wa Amani, Usalama na
Ushirikiano wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na jirani zake.
Pamoja
na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo zilikuwepo nchi za Burundi, Rwanda,
Uganda, Sudani Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kongo,
Angola, Zambia na Tanzania ambazo ni jirani ya Kongo.
Nchi za Ethiopia, Msumbiji na Afrika ya Kusini pamoja na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika zilitia saini kama wadhamini. Ethiopia
kwa nafasi yake ya kuwa Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika na
Msumbiji kwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa
Afrika (SADC).
Nchi wanachama wa Mkutano wa Ukanda wa Maziwa Makuu ziliwakilishwa na Uganda ambayo ni Mwenyekiti wake wa sasa. Afrika ya Kusini ilishirikishwa kwa kuwa taifa kubwa na linalotegemewa katika ukanda wetu.
Mpango huu ni jitihada nyingine ya kusaidia Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ipate amani ya kudumu. Kama
tujuavyo, tangu mwaka 1997 wakati wa vita vilivyosababisha kuondolewa
kwa Rais Mobutu Seseseko mpaka sasa nchi hiyo rafiki na jirani haijapata
amani na utulivu wa kudumu.
Kumekuwepo
jitihada na mipango kadhaa ya kuleta amani ambayo hata hivyo baada ya
muda fulani machafuko hutokea tena na mipango hiyo kuvurugika. Inakadiriwa kuwa takriban watu milioni 5.4 wamepoteza maisha na watu wengi kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi yao. Pia kumekuwepo na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto pamoja na mali nyingi kuharibiwa au kuporwa.
Ndugu Wananchi;
Machafuko
yaliyoanzishwa na waasi wa Kundi la M23 mapema mwaka wa jana ndiyo
sababu ya kuwepo kwa Mpango huu wa sasa tuliotia saini kule Addis Ababa,
Ethiopia tarehe 8 Februari, 2013. Katika Mpango huo
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na jirani zake, Tanzania ikiwemo,
tumekubaliana kutokufanyiana vitendo vinavyohatarisha amani na usalama
wa nchi zetu. Tumeazimia tusifanye hivyo ama moja kwa moja kama nchi au kwa kutumia watu wengine. Aidha, tumekubaliana tusiruhusu watu au vikundi vya watu kutumia nchi zetu kuhatarisha usalama wa nchi nyingine. Kimsingi tumekubaliana kuwa majirani wema. Katika
Mkataba huo, majukumu ya kila nchi yameainishwa vizuri pamoja na yale
ya Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Mashirika ya Kikanda hususan
SADC na ICGLR.
Ndugu Wananchi;
Niliamua
kukubali kushiriki na kutia saini Mpango ule kwa kutambua ukweli kwamba
sisi majirani wa nchi ya Kongo tunao wajibu wa kusaidia kwa kile
tunachoweza.
Wananchi
wa Kongo wameteseka kwa muda mrefu mno hivyo kama Mpango huu
utawasaidia kupata amani na usalama hatuna budi kuunga mkono.
Ni
kwa misingi hiyo hiyo, tulikubali kuchangia kikosi kimoja katika Jeshi
la Kimataifa la kulinda amani huko Mashariki ya Kongo kama ilivyoamuliwa
na Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu mwezi Julai, 2012.
Uamuzi huo umeungwa mkono na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika.
Umoja
wa Mataifa umeamua Jeshi hilo liwe sehemu ya Jeshi la Umoja wa Mataifa
la Kulinda Amani nchini Kongo (MONUSCO) jambo ambalo sote tumeliafiki. Tumepeleka walinzi wa amani Darfur, Sudan na Lebanon, kwa nini tusipeleke Kingo.
Miaka ya nyuma tulishapeleka walinzi wa amani Liberia, Siera Leon na Eritrea.
Ni matumaini yetu kuwa Mpango huu mpya utatekelezwa kwa ukamilifu na kuzaa matunda yaliyokusudiwa.
Kama nchi jirani, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo yenye amani, usalama na utulivu ni jambo lenye maslahi makubwa kwetu.
Ina
maana ya kutokuwa na wakimbizi kutoka nchi hiyo, uharamia katika Ziwa
Tanganyika kutokuwepo na ustawi wa shughuli za kiuchumi na kibiashara
kwa upande wetu na wao. Ni chachu muhimu ya maendeleo ya Mikoa ya pembeni mwa Ziwa Tanganyika na Tanzania kwa jumla.
Uhusiano wa Waislamu na Wakristo
Ndugu wananchi;
Jambo la pili ninalopanga kulizungumzia siku ya leo ni uhusiano wa Wakristo na Waislamu hapa nchini. Kwa
miezi kadhaa sasa tangu mwaka wa jana kumekuwepo na matukio kadhaa
yanayosababisha mifarakano na kupandikiza chuki baina ya waumini wa dini
ya Kikristo na Kiislamu.
Matukio
ya kauli na vitendo vya kudharau dini za wengine, kunajisi vitabu
vitakatifu vya dini hizo, kuchoma moto nyumba za ibada na mzozo kuhusu
nani achinje.
Kumekuwepo na matumizi mabaya ya radio na simu za mkononi na mifumo mingine
ya mawasiliano iliyoeneza maneno na ujumbe wa chuki na vitisho kwa
waumini na viongozi wa dini zetu hizi kubwa hapa nchini.
Kauli
na matendo hayo, katika baadhi ya maeneo yamekuwa chanzo cha uhasama na
magomvi baina ya waumini na hatimaye kusababisha vifo kama ilivyotokea
Buseresere Mkoani Geita na Beit-el-Ras, Zanzibar.
Ndugu zangu;
Watanzania
hatujawahi kuwa hivi, kumetokea nini? Miaka yote Watanzania ni watu
tunaotambua na kuheshimu tofauti za dini zetu mbalimbali tunazoabudu.
Watanzania
ni waelewa na kwa ajili hiyo tumekuwa tunavumiliana kwa tofauti zetu na
ndiyo maana tumekuwa tunaishi pamoja kidugu, kwa umoja na kushirikiana
kwa mambo yote yanayotuhusu maishani isipokuwa wakati kila mmoja
anapoingia kwenye nyumba ya ibada kumuomba Mola kwa misingi na taratibu
ya dini yake.
Watanzania
wa dini zote na makabila tofauti wanaishi nyumba moja, wanasoma pamoja,
wanafanya kazi pamoja kwa udugu, upendo, umoja na ushirikiano. Kuna koo na familia zenye watu wa dini tofauti, wengine Waislamu na wengine Wakristo.
Wapo Waislamu na Wakristo wameoana, wamezaa na wamejukuu na kila mmoja amebakia kuwa mfuasi wa dini yake.
Wapo pia ambao hawakuoa lakini wamezaa watoto na wanashirikiana kulea watoto wao.
Hayo ndiyo maisha ya Watanzania na hiyo ndiyo Tanzania yenye amani na utulivu tuliyozaliwa, kukua na kuishi.
Nawasihi sana Watanzania wenzangu, tuienzi na kuidumisha tunu hii waliyotujengea mababu zetu.
Ndugu Wananchi;
Kuna wenzetu kwa sababu wanazozijua wao na kwa manufaa wanayoyajua wao wanataka kutuvurugia nchi yetu hii nzuri.
Tusiwape nafasi wachochezi hawa kwani hawatutakii mema na wala hawazitakii mema dini zetu na nchi yetu.
Sisi
katika Serikali hatutasita kuwachukulia hatua wale wote wanaochochea
chuki za kidini, wanaodharau vitabu vitakatifu vya dini nyingine na
wanaokejeli dini nyingine.
Nimewakumbusha Polisi na mamlaka husika kote nchini wasifanye ajizi kwenye matukio ya namna hiyo.
Wawachukulie hatua stahiki wale wote wanaohusika. Nimewataka wazingatie msemo wa Kiswahili usemao “ajizi nyumba ya njaa”.
Wachochezi wa mifarakano na chuki za kidini wasipodhibitiwa ipasavyo wataleta maafa kwa Watanzania wasiokuwa na hatia.
Nimewakumbusha Wakuu wa Wilaya na Mikoa kama walinzi wa amani wa maeneo yao ya uongozi, watimize ipasavyo wajibu wao.
Pia
nimewataka Polisi wakamilishe mapema upelelezi wa makosa ya vurugu za
kidini na wahusika wafikishwe haraka kwenye vyombo vya sheria ili iwe
fundisho kwa wengine.
Ndugu Wananchi;
Naendelea
kuwasiliana na viongozi wa dini kuzungumza nao juu ya wajibu wao maalum
wa kuhakikisha kuwa wafuasi wao hawawi chanzo au sehemu ya tatizo na
mifarakano miongoni mwa waumini wa dini mbalimbali nchini.
Hali
kadhalika naitumia nafasi hiyo kuwakumbusha umuhimu wa kuzungumza na
wenzao wa upande mwingine kutatua tofauti au matatizo yanayoathiri
uhusiano mwema baina yao.
Ndugu Wananchi;
Kuna msemo maarufu usemao “mjenga nchi ni mwananchi na mbomoa nchi ni mwananchi”. Naomba tuwe wajenga nchi na kamwe tusikubali kuwa wabomoa nchi.
Hivi tukiibomoa nchi yetu tutakwenda wapi? Tutaishi wapi? Tusikubali kugeuka wakimbizi ndani ya nchi au nje ya nchi yetu.
Kwa
mara nyingine tena, napenda kutumia nafasi hii kuwapa mkono wa pole
makanisa, familia, ndugu na jamaa wote wa Mchungaji Kachila na Padri
Mushi. Sote tunafahamu machungu waliyonayo kwa kuondokewa na wapendwa wao.
Serikali na wapenda amani wote nchini wapo pamoja nanyi katika kipindi hiki kugumu.
Vile
vile natoa rambirambi zangu nyingi kwa waumini wote wa Kanisa la
Pentekoste Assemblies of God na Kanisa Katoliki Tanzania kwa kuondolewa
ghafla na viongozi wao.
Tuzidi kumwomba Mwenyezi Mungu azipumzishe kwa amani roho za viongozi wetu. Amin.
Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne Mwaka 2012
Ndugu wananchi;
Tarehe 18 Februari, 2013 Baraza la Mitihani la Taifa lilitangaza matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne ya mwaka 2012. Wanafunzi 397,132 walifanya mtihani huo na kati ya hao, waliofaulu ni 126,851 yaani sawa na asilimia 34.5. Wanafunzi 240,903ambao ni sawa na asilimia 65.5hawakufaulu mtihani huo.
Kwa ulinganifu, matokeo hayo ni mabaya kuliko matokeo mengine ya mtihani huo ya miaka ya hivi karibuni.
Mwaka 2011, jumla ya wanafunzi 336,782walifanya mtihani huo na waliofaulu walikuwa asilimia 53.6 na ambao hawakufaulu kabisa walikuwa asilimia 46.4. Mwaka 2010 jumla ya wanafunzi 352,045 walifanya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne, asilimia 50.4 ya wanafunzi hao walifaulu na asilimia 49.6 ya wanafunzi hawakufaulu.
Ndugu Wananchi;
Matokeo ya mitihani ya kidato cha nne mwaka 2012, yameshtua na kufadhaisha watu wengi nchini na kwa sababu stahiki kabisa.
Kwanza, kwamba kiwango cha kufaulu kimeporomoka sana, tena ghafla, kutoka asilimia 53.6 mwaka 2011 hadi asilimia 34.5 mwaka 2012. Hili ni anguko la asilimia 19.1 ambalo, kwa kila hali, ni kubwa sana.
Pili,
kwamba hata shule zinazofahamika kuwa na historia ya kufaulisha vizuri
kama vile seminari, shule za watu binafsi, za mashirika ya dini na
sekondari kongwe za Serikali ambazo hazina matatizo kama ilivyo kwa zile
sekondari za Kata, nazo safari hii hazikupata mafanikio kama ilivyo
kawaida yao.
Nazo zimejikuta zikiwa na idadi ya vijana waliopata daraja la kwanza, la pili na la tatu ikipungua wakati waliopata daraja la nne na waliofeli wakiongezeka.
Isitoshe na kiwango cha ufaulu wa vijana umepungua pia. Mwaka 2010 wanafunzi 10 bora wote walikuwa wamefaulu daraja la kwanza la alama au pointi 7.
Mwaka 2011 katika wanafunzi 10 bora wanane walipata daraja la kwanza kwa alama 7 na wawili alama 8. Mwaka 2012 katika wanafunzi 10 bora, watatu walipata daraja la kwanza kwa alama 9, watatu alama 10 nawawili alama 11.
Ndugu Wananchi;
Haya ndiyo mambo yanayozua maswali kwa watu wengi yanayohitaji kupatiwa majawabu ya uhakika. Kulikoni mwaka 2012? Ndiyo
msingi wa uamuzi wa Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda, kuamua kuunda Tume
ya kuliangalia suala zima la mitihani ya mwaka 2012 na matokeo yake. Hali hii haijawahi kutokea katika miaka ya hivi karibuni.
Ni suala muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu, hivyo lazima ukweli wake ujulikane kwa uhakika.
Hii
itawezesha Serikali na wadau wengine kuchukua hatua stahiki kurekebisha
mambo mapema iwezekanavyo ili hatimaye mambo yawe mazuri siku za usoni.
Tusipofanya hivyo mambo yanaweza kuwa mabaya zaidi na lawama zinaweza kuwa kubwa zaidi kwa Serikali.
Ndugu Wananchi;
Hivi sasa kunatolewa mawazo lukuki kuhusu sababu za kwa nini matokeo yamekuwa mabaya.
Wapo wanaodhani kuwa lipo tatizo katika utungaji wa mitihani, usahihishaji wake au kutoa maksi kwa watahiniwa.
Wapo wanaodhani walimu hawawajibiki ipasavyo au baadhi yao kutokumudu masomo wanayofundisha.
Wapo
wanaofikiria kuwa wanafunzi hawako makini katika kufuatilia masomo na
wazazi hawajali kufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni.
Wapo wanaoinyooshea kidole Serikali kwa sera, mitaala na uwekezaji usiokidhi mahitaji ya maendeleo ya elimu.
Wapo wanaofikiria kuwa Serikali kushindwa kuongeza mishahara ya walimu kwa asilimia 100 kama walivyotaka imechangia.
Orodha ni ndefu, ali mradi kila mtu ana mawazo yake.
Na sisi katika Serikali hatuwezi kuwa tunadhani kwa sababu tunayo dhamana maalum.
Lazima tujue ukweli kwa uhakika na ndiyo maana kuna umuhimu wa Tume. Naomba kila mtu mwenye mawazo yake ayafikishe kwenye Tume hiyo hapo itakapoundwa ili tupate jawabu muafaka la tatizo hili.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kuwahakikishia kuwa sisi katika Serikali tumetoa kipaumbele cha juu
sana kwa elimu na kwamba hakuna upungufu wa utashi kwa upande wangu na
wenzangu wote Serikalini. Ndiyo maana tumeguswa sana na matokeo haya.
Bajeti ya elimu ya shilingi trilioni 3.6 ambayo ni sawa na asilimia 24 ya bajeti yote ya Serikali ndiyo kubwa kuliko zote.
Kwa ajili hiyo imetuwezesha kuendelea kukabili mahitaji na changamoto za upanuzi mkubwa wa elimu ya sekondari na elimu ya juu.
Bado hatujazimaliza changamoto zote na kwamba bado tuna kazi kubwa mbele yetu, lakini mafanikio yanaendelea kupatikana.
Tutaendelea
kutoa kipaumbele cha juu kwa elimu mpaka hapo itakapofikia mahali
kwamba matatizo makubwa yatakapokuwa yamepungua sana.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Ibariki Afrika!
Nashukuru kwa kunisikiliza!