tangazo
Majid Mjengwa.
MWANDISHI
wa safu katika magazeti mbalimbali nchini, Majid Mjengwa amekamatwa na
polisi kwa tuhuma za kuhusika na tukio la kushambuliwa kwa Mwenyekiti
wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda.
Habari
zilizoufikia mtandao huu jana mchana na baadaye kuthibitishwa na
polisi zinasema Mjengwa alikamatwa muda wa asubuhi na kwamba alikuwa
akihojiwa na makachero wa jeshi hilo hadi alasiri kuhusu tukio la
kuteswa kwa Kibanda.
Msemaji Mkuu wa Polisi Advera Senso alisema kwamba:
“Ni
kweli kwamba tunaye, tunaendelea kumhoji, tunachoomba ni kwamba mtupe
nafasi ili tufanye kazi yetu na kukiwa na jambo lolote tutawajulisha.”
Hata
hivyo, Senso hakuwa tayari kueleza kwa undani muda aliokamatwa Mjengwa
wala sababu za kukamatwa na kuhojiwa kwake, lakini chanzo chetu ndani
ya Jeshi la Polisi kilithibitisha kwamba pamoja na mambo mengine
kuhojiwa kwake kulihusu uteswaji wa Kibanda.
Jumatatu
wiki hii, Kaimu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Nchini, Issaya Mngulu
alisikika akizungumza na Kituo cha Radio One cha Dar es Salaam kwamba
kesho Jumatatu (April 15, 2013) polisi watatoa taarifa rasmi ya hatua
waliofikia katika upepelezi wa kesi ya Kibanda.
Kwa
upande wake Mia Mjengwa ambaye ni mke wa Mjengwa, alisema mumewe
alipata wito kutoka polisi makao makuu Alhamisi na kwamba juzi Ijumaa
alisafiri kutoka Iringa kwenda Dar es Salaam kuitikia wito huo.
“Ninachojua
ni kwamba aliitwa kwenda polisi na leo (jana) alinipigia simu kama saa
7:00 mchana na aliniarifu kwamba yupo polisi, sasa tangu wakati huo
sijaongea naye tena na wala simu zake hazipatikani,” alisema Mia na
kuongeza: “Kwa hiyo mimi kwa kweli sifahamu kwamba anahojiwa kwa sababu
gani.”
Taarifa
za kukamatwa kisha kuhojiwa kwa Mjengwa ambaye pia ni mmiliki wa
Mjengwa Blog, zimekuja siku chache tangu msaidizi wake katika Blog
hiyo, Joseph Ludovick akamatwe, kuhojiwa kisha kufikishwa mahakamani
kwa tuhuma za ugaidi.
Ludovick
alifikishwa mahakamani pamoja na Mkurugenzi wa Usalama wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Willifred Lwakatare wakikabiliwa na
tuhuma za ugaidi na kupanga kumteka Mhariri Mtendaji wa Mwananchi,
Dennis Msacky.
Kuteswa Kibanda.
Machi
5, mwaka huu saa 5.30 usiku, Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa
Magazeti ya Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, alinusurika kifo baada
ya kuvamiwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake kisha kupigwa na
kujeruhiwa vibaya.
mwananchi
mwananchi