tangazo
MBUNGE
wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy (CCM) alhamisi ya wiki hii aliwavunja mbavu wabunge
baada ya kuwasuta wabunge wanaojichubua ngozi akiwaambia wanaohitaji
ngozi nyeupe wamuone.
Ameitaka
pia Serikali isiishie kukamata waingizaji wa vipodozi hatari, bali pia
watumiaji wakiwemo wabunge. Kessy alisema Serikali inapaswa ikamate na
watumiaji wa vipodozi hivyo kama ambavyo huwa inafanya kwa waingizaji
na watumiaji wa dawa za kulevya.
Akichangia
wakati wa kujadili vifungu kabla ya kupitisha bajeti ya Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii juzi, alisema inashangaza kuona katika meza za
kujipodoa za wanawake wakiwemo wabunge, vimejaa vipodozi lakini
serikali haiendi kuwakamata.
Alisema
hata bungeni wapo wanawake wanaotumia dawa za kubadilisha sura kiasi
kwamba wakienda vijijini kwao, ndugu zao wanawakimbia, lakini Serikali
haiwakamati.
“Wanajiharibu
sura huwezi kujua ni raia wa nchi gani; unashindwa kujua hawa ni
Wachina, Wajapani ukianzia humu humu bungeni,” alisema Kessy na
kusababisha kicheko bungeni.
Mbunge
huyo aliendelea kuwavunja mbavu pale ambapo alisema wanaotaka
kubadilisha rangi zao, wawaone watu weupe kama yeye wawape mbegu.
Kessy
alitoa utani huo baada ya Naibu Spika, Job Ndugai kumtania akisema “Na
wewe ni matokeo ya vipodozi hivyo,” akimaanisha weupe wa Mbunge huyo.
“Nashauri
wanaotaka kubadilisha rangi zao watuone sisi tuwape mbegu,” alisema na
kuendelea kusababisha ukumbi mzima wa bunge ulipuke kwa kicheko.
Akijibu
hoja hiyo, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi
alisema jukumu la wizara yake ni kuangalia usalama wa vipodozi na
haijihusishi kujua nani anatumia na nani hatumii.
Alisema
wajibu wake ni kuhakikisha vipodozi vinavyoingia nchini vinakuwa na
viwango. Alisema wanaotumia ni hiari yao kwa kuwa Wizara ikiingilia,
utakuwa ni ubaguzi wa kijinsia.
Hata hivyo, Dk Mwinyi alisema watumiaji wanapaswa kuhakikisha kwamba vipodozi husika vimethibitishwa usalama wake.