tangazo
Matokeo ya mtihani wa kidato cha sita yaliyotarajiwa kutangazwa mwezi huu yatachelewa ili kutoa nafasi kwa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), kurekebisha matokeo mabaya ya mitihani kidato cha nne ya mwaka jana yaliyofutwa na serikali mwezi huu.
Matokeo ya kidato cha sita ambayo huwa yanatangazwa mwanzoni mwa mwezi Mei mpaka sasa hayajatolewa na kwamba hayatatangazwa mpaka matokeo mapya ya kidato cha nne yatakaporekebishwa rasmi.
Alipoulizwa
juu ya suala hilo, Naibu Waziri wa Elimu na Mfunzo ya Ufundi
Philipo Mulugo alisema ingawa wakati huu ndio unaopaswa yatangazwe
matokeo ya kidato cha sita haitafanyika hivyo hadi yatangazwe matokeo
mapya ya kidato cha nne baada ya kufutwa.
Hata
hivyo, akasema huenda yakatolewa pamoja au yakafuata wakati mwingine
lakini mara baada ya kukamilisha kazi ya kurejea na kusahihisha
matokeo ya kidato cha nne.
"Siyo kwamba yamechelewa kwani muda wa kujiunga na chuo ni Septemba hivyo haitawaathiri kwa hilo," alisema Mulugo.
Kuhusu
hatma ya wanafunzi wa kidato cha nne ambao wapo mashuleni wanaendelea
na masomo ya kidato cha sita, alisema kama kutakuwa na wanafunzi ambao
wapo madarasani shule zilizowasajili zitakuwa hazijafuata mfumo wa
elimu unavyoelekeza.
Alifafanua
kuwa mfumo wa elimu kwa kidato cha nne ulibadilishwa na kwamba endapo
mwanafunzi akifaulu anatakiwa kujiunga rasmi kidato cha sita Julai na
si vinginevyo.
Alisema
licha ya ucheleweshaji wa matokeo hali hiyo haikuwaathiri wanafunzi
hao kwa kuwa ratiba ya kwenda masomoni haijaanza kwa mujibu wa
kalenda ya shule ya serikali.
Serikali
ilifuta matokeo ya kidato cha nne ya 2012 na kuiagiza Necta kuyaandaa
upya kwa kutumia utaratibu wa usahihishaji na upangaji madaraja
uliotumiwa mwaka 2011
Taarifa
ilisema mfumo uliotumika mwaka jana na kusababisha wanafunzi
kushindwa vibaya haukufanyiwa utafiti na maandalizi ya kutosha kabla ya
kutumika.
Matokeo hayo yaliyotangazwa mwezi Februari mwaka huu yalionyesha kuwa asilimia 60 ya wanafunzi walishindwa mtihani.