tangazo
AMA kweli pombe mwanaharamu, ukimkuta mtu anasifia pombe basi mpe pole yake kwani hayo ni matumizi mabaya ya akili alizopewa bure na Mwenyezi Mungu, hali imejidhihirisha kwa mkazi mmoja wa Kwimba, Mwanza, Nhende Ng’wanandilima (35) aliyeliwa na fisi sehemu kubwa ya uso wake.
Kwa mujibu wa mashuhuda, wakati kijana huyo akiliwa, alipiga kelele zilizofika kwenye kijiji hicho ambapo majirani walifika na kumnusuru kisha kukimbiza Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa matibabu zaidi.
Kwa mujibu wa Nhende, hali aliyonayo kwa sasa inamnyima raha kwani amekuwa kilema, kitu ambacho hakufikiria kinaweza kutokea maishani mwake.
Hata hivyo, alieleza kuwa daktari mashuhuri wa masuala ya koo na mfumo wote wa ‘ogani’ za fahamu amempa matumaini baada ya kumuahidi kumtengeneza upya sehemu zote zilizoliwa na fisi huyo.
“Hali hii si nzuri kwani napata maumivu makali, sikuwahi kujua kama fisi anaweza kumla binadamu hivi, pia namshukuru Mungu nimekatwa nyama za mapaja Jumatatu ya wiki hii ili kusukwa upya kwa mfumo wote wa sura yangu, Dokta Gliyoma ndiyo mkombozi wa maisha yangu.
“Nawashauri vijana wenzangu waache pombe kwani ina madhara makubwa kama niliyoyapata mimi,” alisema.