tangazo
Nakushukuru sana Mheshimiwa Spika kwa kukubali ombi langu na
kutenga muda wenu ili niweze kuzungumza na Wabunge wa Bunge lako Tukufu
kuhusu masuala muhimu kwa uhai, ustawi na maendeleo ya nchi yetu na watu
wake.
Mheshimiwa Spika;
Nimeambiwa kuwa taarifa ilipotolewa kuwa ninaomba kuja
kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge, kumekuwepo na dhana mbalimbali. Wapo
waliodhani kuwa nakuja kuzungumzia mchakato wa kuunda Katiba mpya na
hasa matukio ya wiki chache zilizopita. Wapo waliodhani nakuja
kuzungumzia “Operesheni Tokomeza”. Tena wapo waliokwenda mbali na
kufikiria kuwa nakuja kuwakaripia Waheshimiwa Wabunge waliotoa maoni yao
kuelezea kasoro zilizojitokeza katika utekelezaji wa Operesheni hii
muhimu. Na wapo pia waliodhani ninakuja kuzungumzia ushiriki wa majeshi
yetu ya Tanzania katika Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa
nchini Kongo.
Mheshimiwa Spika;
Hayo si makusudio yangu. Kinachonileta mbele ya Bunge
lako Tukufu ni kuzungumzia Jumuiya ya Afrika Mashariki na mustakabali wa
Tanzania katika Jumuiya hiyo. Lakini, kwa sababu ya umuhimu wa masuala
hayo niliyoyataja na rai niliyopewa kuwa niyasemee japo kidogo.
Nimeona ni vyema nifanye hivyo.
Mheshimiwa Spika;
Kuhusu mchakato wa Katiba mpya, napenda kusema kuwa tumefikia
hatua nzuri katika utekelezaji wake. Kama mjuavyo Tume ya Mabadiliko ya
Katiba imekamilisha, kwa mafanikio, hatua ya mwanzo ya kusikiliza maoni
ya wananchi kuhusu Katiba wanayoitaka. Pia walishatoa Rasimu ya Kwanza
ya Katiba na kukamilisha mchakato wa Mabaraza ya Katiba.
Kinachosubiriwa kwa hamu na sisi wote, ni Rasimu ya Pili ya Katiba
ambayo inatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 15 Desemba 2013 au kabla ya
hapo.
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa Bunge lako Tukufu, tunategemea kupata mambo
mawili kutoka kwenu yatakayowezesha mchakato kutekelezwa vizuri katika
hatua zinazofuata. Jambo la kwanza ni kutungwa kwa Sheria ya Kura ya
Maoni na pili kufanyika kwa marekebisho ya nyongeza ya Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba kuhusu Bunge Maalum ili kuboresha utekelezaji
wake. Baada ya Bunge kukamilisha kazi yake hiyo itafuatia uteuzi wa
Wajumbe wa Bunge Maalum ili kazi ya kujadili Rasimu ya Pili ya Katiba
ifanyike na kutupatia Rasimu ya Mwisho. Rasimu ambayo ikikubaliwa na
wananchi katika Kura ya Maoni itakayofanyika wakati wo wote mwakani,
tutakuwa tumepata Katiba Mpya. Hivi sasa katika Serikali tunaendelea
kufanya tafakuri na tunachukua hatua za kuwezesha Bunge Maalum na Kura
ya Maoni kufanyika kwa mafanikio.
Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika;
Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako
Tukufu kuwa sikukasirishwa na maoni yao kuhusu madai ya kuwepo kasoro
katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. Shabaha ya Operesheni hii ni
kuokoa maliasili za misitu na wanyamapori dhidi ya uvunaji haramu ambao
umefikia kiwango kinachotishia kutoweka kwa raslimali hizo. Kwa kweli
hali inatisha. Miti inakwisha na ndovu na faru wanaangamia.
Mheshimiwa Spika;
Wakati, tunapata Uhuru Tanzania ilikuwa na ndovu waliokadiriwa kuwa takribani 350,000. Lakini, kwa sababu ya ujangili uliokithiri katika miaka ya 1970 na 1980 ilipofika mwaka1989 kulikuwa na ndovu wapatao 55,000 tu.
Ilipofikia hali hiyo Serikali ikaanzisha Operesheni Uhai iliyohusisha
Jeshi la Ulinzi na kuongozwa na Meja Jenerali John Walden (ambaye sasa
ni marehemu) kuendesha mapambano dhidi ya majangili. Kutokana na hatua
hiyo na uamuzi wa Shirika linalosimamia biashara ya wanyama walioko
kwenye hatari ya kutoweka (CITES) kupiga marufuku biashara ya pembe za
ndovu duniani, idadi ya ndovu nchini iliongezeka na kufikia 110,000 mwaka 2009.
Tumewaomba Fankfurt Zoological Society ambao ni wabia wetu katika
uhifadhi wa wanyama pori kwa miaka mingi wafanye sensa maalum ya ndovu
katika Hifadhi ya Selous na kote nchini ili tujue hali halisi ikoje.
Kazi hiyo inaendelea hivi sasa.
Mheshimiwa Spika;
Baada ya mwaka 2009 kumezuka wimbi jipya, tena la nguvu
kubwa, la kuua ndovu na faru nchini na kwingineko katika Bara la Afrika
ambako wanyama hao wapo. Idadi kubwa ya meno ya ndovu yaliyokamatwa na
yanaoendelea kukamatwa nchini na kwingineko duniani inathibitisha ukweli
huo. Kwa mfano, kati ya mwaka 2010 na Septemba, 2013, hapa nchini, kwa
jitihada zetu vipande 3,899 vya pembe za ndovu vyenye uzito wa kilo 11,212 na vipande 22 vya pembe za ndovu zilizochakatwa zenye uzito wa kilo 3,978vilikamatwa. Aidha, katika kipindi hicho vipande 4,692 vya pembe za ndovu vilivyotokea Tanzania vyenye uzito wa kilo 17,797vilikamatwa nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika;
Kama nilivyokwisha sema hapo awali matatizo ya kuuawa kwa
wingi kwa ndovu na faru lipo pia katika nchi nyingine Afrika zenye
wanyama hao. Nchi za Gabon, Kenya, Afrika ya Kusini, Jamhuri ya Afrika
ya Kati, Uganda, Zimbabwe, Zambia na nyinginezo nazo zinakabiliwa na
matatizo kama yetu. Tatizo limekuwa kubwa kiasi cha kuifanya Jumuiya ya
Kimataifa kushtuka na kuamua kuingilia kati kwa namna mbili. Kwanza
kuunga mkono juhudi za uhifadhi wa ndovu na faru katika nchi zenye
wanyama hao. Na, pili, kuchukua hatua thabiti kudhibiti biashara ya
meno ya ndovu duniani. Ni ukweli ulio wazi kuwa kama hakutakuwepo na
wanunuzi wa meno ya ndovu na faru hakuna ndovu au faru atakayeuawa.
Mheshimiwa Spika;
Kutokana na ukweli ulivyo uamuzi wetu wa kuendesha Operesheni
Tokomeza ni sahihi kabisa. Manufaa yaliyopatikana baada ya Operesheni
Uhai ya mwaka 1989 yanatupa imani kuwa na safari hii pia
tutafanikiwa. Tusipochukua hatua kama hii sasa ni sawa na kuwapa kibali
majangili waendelee kumaliza ndovu na faru nchini. Hakika wanyama hao
watakwisha. Itakuwa ni aibu kubwa kwetu na historia itatuhukumu vibaya.
Mheshimiwa Spika;
Tumeyasikia maelezo ya Wabunge kuhusu kasoro mbalimbali
zilizojitokeza katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. Nawaahidi
kuwa tutayafanyia kazi. Serikali imeahirisha kwa muda Operesheni hii
ili kujipa muda wa kurekebisha kasoro hizo na kujipanga upya. Watendaji
wasiokuwa waadilifu na wale wasiokuwa waaminifu wataondolewa.
Halikadhalika, kasoro za kimfumo nazo zitasahihishwa ili tutakapoanza
upya Operesheni itekelezwe kwa mafanikio yaliyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika;
Miongoni mwa mambo yaliyozungumzwa kwa uchungu ni
ukamataji wa mifugo iliyokutwa kwenye mapori ya hifadhi za wanyama na
vitendo vibaya walivyofanyiwa wenye mifugo na mifugo yenyewe. Narudia
kusisitiza kuwa taarifa zote hizo zitafanyiwa kazi na waliohusika
watachukuliwa hatua zipasazo. Pamoja na hayo, napenda kuwakumbusha
ninyi watunga sheria wetu kuwa sheria ya hifadhi za wanyamapori
hairuhusu mifugo kuchungwa katika maeneo ya hifadhi.
Naomba tuwakumbushe wananchi tunaowaongoza wajiepushe na kufanya
hivyo. Ni uvunjifu wa Sheria za nchi. Naomba pia, wananchi waelimishwe
ili wajue kuwa wakifanya hivyo na kukutwa katika maeneo hayo na mifugo
yao kuna adhabu iliyotamkwa kwenye sheria. Hivyo tusiwalaumu wala
kuwaona maafisa wanyamapori kuwa ni watu wabaya. Wanatekeleza Sheria
iliyotungwa na Bunge hili. Pale wanapotenda visivyo tuseme,
watawajibishwa ipasavyo.
Jeshi la Umoja wa Mataifa Kongo
Mheshimiwa Spika;
Mapema mwaka huu (2013) Umoja wa Mataifa uliomba nchi
yetu ichangie kikosi kimoja cha wanajeshi katika Brigedi Maalum
iliyoundwa na Umoja huo kuongeza nguvu ya kudhibiti waasi Mashariki ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Lengo la msingi ni kuiwezesha nchi
hiyo kupata amani ya kudumu ambayo imekosekana kwa muda mrefu kutokana
na kuibuka kwa uasi mara kwa mara.
Mheshimiwa Spika;
Tulikubali, kwani hata kabla ya kuombwa na Umoja wa
Mataifa tulishakubali maombi kama hayo yaliyotolewa kwenye Mkutano wa
Nchi za Maziwa Makuu. Ni miezi saba (tangu Aprili) sasa tangu wanajeshi
wetu waende Kongo na wamekuwa wanatekeleza majukumu yao vizuri tena kwa
weledi na nidhamu ya hali ya juu. Sifa hiyo kwa wanajeshi wetu imekuwa
inatolewa na viongozi wa juu wa Umoja wa Mataifa, viongozi wa juu wa
Jeshi la Umoja wa Mataifa Kongo (MONUSCO) na viongozi wa juu wa Serikali
ya Kongo.
Mheshimiwa Spika;
Majeshi ya Umoja wa Mataifa hupewa majukumu na mamlaka ya
namna mbili. Yapo yanayopewa jukumu la kulinda amani tu. Wanajeshi
wake huwa hawapewi majukumu ya kimapigano na hata pale wanaposhambuliwa
wanatakiwa kujihami tu. Kwa kawaida majeshi yenye jukumu hili hupelekwa
mahali ambapo kumekuwepo na makubaliano ya kuacha mapigano.
Wanapelekwa kusaidia kuona Mkataba unatekelezwa ipasavyo.
Aina ya pili ni ile ya majeshi yanayopelekwa mahali ambapo hakuna
amani hivyo wanapewa jukumu la kuchukua hatua za kufanya amani
ipatikane. Majeshi haya hupewa mamlaka ya kutumia nguvu ya kijeshi
dhidi ya wanaosababisha amani ikosekane kama ni lazima kufanya hivyo.
Maana yake ni kwamba wanayo ruhusa kuingia katika mapigano dhidi ya watu
au vikundi vinavyovuruga amani. Tofauti na wenzao wa kundi la kwanza,
wanajeshi wa kundi la pili wako kwenye hatari zaidi ya kupoteza maisha
au kujeruhiwa kuliko wenzao ingawaje wapo wengi nao wameuawa na
kujeruhiwa.
Mheshimiwa Spika;
Wanajeshi wetu wamekwenda Kongo chini ya utaratibu huu wa pili
ambao unahusu kuingia kwenye mapigano dhidi ya waasi kama hapana budi
kufanya hivyo. Wametekeleza majukumu yao vyema na kwa ujasiri mkubwa
na weledi wa hali ya juu. Bahati mbaya tumepoteza vijana wetu watatu
shupavu. Daima tutawakumbuka na tutawaenzi ipasavyo mashujaa wetu
hawa. Tuzidi kuwaombea kwa Mola awape mapumziko mema. Ameen.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Spika, napenda kutumia nafasi hii
kumpongeza Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa
mafanikio ya kihistoria waliyoyapata hivi majuzi dhidi ya waasi wa M23.
Tunamtakia yeye na wananchi wa Kongo kila la heri katika kazi ngumu
iliyo mbele yao ya kujenga upya eneo hilo na kujenga mahusiano mapya
miongoni mwa watu wa Kongo. Pia nawapongeza sana wanajeshi wa Brigedi
Maalum ya Umoja wa Mataifa kwa kazi nzuri waliyoifanya iliyowezesha
mafanikio kupatikana. Wanajeshi hao ni kutoka Afrika Kusini, Tanzania
na Malawi wanaoongozwa na Brigedia Jenerali James Aloisi Mwakibolwa wa
JWTZ.
Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mheshimiwa Spika;
Kama nilivyosema awali, haya mambo matatu siyo hasa
makusudio yangu nilipoomba kuja kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge wetu.
Nimeyachomekea tu kwa sababu ya umuhimu wake katika jamii kwa wakati
tulio nao. Jambo lililonileta hapa leo ni kuzungumzia hali ilivyo sasa
katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na nafasi ya Tanzania katika Jumuiya
hiyo. Nimeona nifanye hivyo kutokana na maswali mengi ambayo Watanzania
wanajiuliza kufuatia matukio ya hivi karibuni ya viongozi wa nchi tatu
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaani Uganda, Rwanda na Kenya
kukutana bila ya ushiriki wa viongozi wa Tanzania na Burundi. Viongozi
wenzangu hao wamefanya mikutano mitatu yaani: tarehe 24-25 Juni, 2013
mjini Entebbe, Uganda; tarehe 28 Agosti, 2013 mjini Mombasa, Kenya; na
tarehe 28 Oktoba, 2013 mjini Kigali, Rwanda.
Mheshimiwa Spika;
Naomba kwanza niweke wazi jambo moja, kwamba nchi mbili
wanachama au zaidi hazikatazwi kuwa na makubaliano ya ushirikiano katika
kufanya mambo mbalimbali. Hata sisi Tanzania tunao ushirikiano wa
namna hiyo na nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Lakini, nchi wanachama zinatakiwa kufanya hivyo kwa yale mambo ambayo
hayako kwenye shughuli za Jumuiya kwa maana kwamba hayamo katika Mkataba
au Itifaki au hakuna uamuzi wa msingi uliofanywa na vikao au taasisi za
Jumuiya kuyashughulikia. Pia, tunaweza kufanya hivyo kwa mambo ambayo
yalishaamuliwa na Jumuiya yatekelezwe na ruhusa imetolewa kwa nchi yo
yote iliyokuwa tayari kutekeleza ama peke yake au kwa kushirikiana na
nchi nyingine.
Mheshimiwa Spika;
Kwa mujibu wa matamko ya pamoja (Communique) yaliyotolewa baada ya mikutano hiyo, kuna mambo yapatayomanane ya
msingi yaliyoamuliwa kufanywa na nchi hizo kwa lengo la kuendeleza
utengamano wa nchi hizo wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mambo
hayo ni haya yafuatayo:
(1) Kujenga reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Kampala, Kigali na Bujumbura.
(2) Ujenzi wa Bomba la Mafuta la kutoka Kenya hadi Uganda na Sudani ya Kusini.
(3) Kujenga Kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda.
(4) Kuanzisha Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutekeleza vipengele vyote;
(5) Kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki na kwamba itaundwa Kamati ya kuandaa rasimu ya Katiba ya Shirikisho.
(6) Kuharakisha uanzishwaji wa Visa ya pamoja ya Utalii
ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (Single East African Community Tourist
Visa);
(7) Kuandaa utaratibu wa kutumia vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria katika nchi zao; na
(8) Kuongeza uzalishaji na usambazaji wa umeme.
Mheshimiwa Spika;
Ni dhahiri kwamba orodha hiyo imechanganya mambo yale
ambayo ni ya Jumuiya na yale yasiyo ya Jumuiya. Kwa mfano, mambo manne kati ya hayo manane hayamo
kwenye masharti ya kutokufanyika bila ya kuihusisha au kupata ridhaa ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki. Jambo la kwanza ni uzalishaji na
usambazaji wa umeme. Ni kweli kwamba tunao mkakati wa kuwa na akiba ya
pamoja ya nguvu ya umeme (East African Power Pool). Hata hivyo, bado
jukumu la kuzalisha na kusambaza umeme huo limeachiwa nchi wanachama
zenyewe kuamua. Lakini, hivi ndugu zetu hawa wanao muhali kuishirikisha
Tanzania katika mpango ambao kimsingi umebuniwa na Jumuiya ya Afrika
Mashariki ambayo sote ni wanachama?
Jambo la pili, ni ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta nchini
Uganda. Hili si suala la Jumuiya bali la nchi ya Uganda kuamua yenyewe
peke yake au kwa kushirikiana na wadau wengine. Rais Yoweri Museveni
alituarifu mpango huo na sote tuliupokea kwa furaha kwamba sasa tutapata
mafuta karibu na nyumbani. Alitualika kushiriki katika ujenzi wake
sijui sasa amebadili mawazo kwamba Tanzania siyo muhimu.
Mheshimiwa Spika;
Jambo la tatu ni ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Kenya hadi Sudani
ya Kusini na Uganda. Hili si jambo linalobanwa na masharti ya Jumuiya.
Ni juu ya nchi hizi tatu kuamua kufanya ili kuwezesha mafuta yao kufika
kwenye masoko. Hata hivyo, nimeambiwa kuwa Jumuiya imeshazungumzia
bomba la mafuta kutoka Eldoret hadi Uganda, Rwanda na Burundi kuwa nalo
lifike Tanzania kupitia upande wa Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.
Inaelekea mpango huo sasa haupo maana hatujausikia kutajwa katika ujenzi
wa bomba hilo.
Mheshimiwa Spika;
Jambo la nne ni ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mombasa – Kampala –
Kigali – Bujumbura. Hili nalo hatuna tatizo nalo. Si mradi wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki, ni jambo lililo chini ya mamlaka ya nchi wanachama
husika. Hata hivyo, ni vyema kutambua ujenzi wa miundombinu ya reli,
barabara na usafiri wa anga na majini kuunganisha nchi za Afrika
Mashariki ni miongoni mwa mambo ya kipaumbele cha juu yanayoshughulikiwa
na Jumuiya yetu. Jumuiya hutengeneza mikakati ya pamoja na ndiyo maana
tuna East African Railway Masterplan, tuna East African Road Network,
na tuna Lake Victoria Development Programme kwa ziwa Victoria.
Kwa ajili hiyo, nilitegemea kuwa reli ya kutoka Mombasa hadi Kigali
na Juba ingekuwa na tawi linalounganisha reli hiyo na reli ya Tanzania
kama ilivyo reli ya Moshi – Voi – Taveta aliyotuachia mkoloni.
Tulitegemea hivyo kwa minajili ya kuunganisha soko la Afrika Mashariki
ambapo naamini Tanzania ni mdau muhimu. Lakini inaelekea kwa maoni ya
wenzetu hivyo sivyo.
Mheshimiwa Spika;
Lazima nikiri kuwa inashangaza na tunayo kila sababu ya kuuliza kwa
nini wenzetu wameamua kufanya hivi. Kumetokea nini toka tukutane pale
Arusha Aprili 28, 2013 na Juni 24, 2013 walipokutana kuamua kufanya
mambo ya kujenga na kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki kwa
kubaguana, Haijawahi kuwa hivi kabla.
Mheshimiwa Spika;
Katika mambo manne yaliyosalia ambayo yaliamuliwa na
kuwekewa utaratibu wake wa utekelezaji na Jumuiya ya Afrika Mashariki
mawili hatuna maneno nayo. Mambo hayo ni matumizi ya vitambulisho vya
taifa kama hati ya kusafiria na Visa ya Pamoja ya Utalii kwani tuliamua
kwa pamoja kuwa nchi wanachama zilizokuwa tayari waanze. Lakini, kwa
upande wa kuanzishwa kwa Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha (Single
Customs Territory) na Shirikisho la Afrika Mashariki tunadhani wenzetu
wamekiuka uamuzi wetu wa pamoja.
Mheshimiwa Spika;
Katika Mkutano Maalum wa 11 wa Wakuu wa Nchi wanachama
uliofanyika tarehe 28 Aprili, 2012 Jijini Arusha, tulipokea na kuridhia
mapendekezo ya kuanzisha Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha (Single
Customs Territory). Kwa mujibu wa mapendekezo hayo kila nchi mwanachama
itasimamia shughuli zake za kiforodha na kukusanya mapato yake kama
ilivyo sasa. Hata hivyo, kwa bidhaa zinazopitia nchi moja kwenda nchi
nyingine mwanachama, ukaguzi na ukusanyaji wa mapato utafanyika katika
kituo cha kwanza bidhaa hizo zinapoingilia. Mapato hayo yatawasilishwa
kwa nchi husika baada ya kuthibitisha kuwa bidhaa zilivuka mpaka.
Mheshimiwa Spika;
Kutokana na uamuzi huo, Wakuu wa Nchi waliagiza Baraza la Mawaziri
kuunda Kikosi Kazi cha kujadiliana na kuandaa utaratibu wa utekelezaji
wa mfumo huo. Taarifa ya kikosi kazi inatakiwa kutolewa katika Mkutano
wa 15 wa Wakuu wa Nchi utakaofanyika Kampala, Uganda tarehe 30 Novemba,
2013. Iweje leo nchi tatu wanachama ziamue peke yao kuanza kutekeleza?
Wanatekeleza nini na kwa nini wafanye hivyo?
Mheshimiwa Spika;
Kuhusu Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki hadithi
yake inafanana na hii ya Himaya ya Forodha. Katika Mkutano wa 14 wa
Wakuu wa Nchi wanachama uliofanyika tarehe 30 Novemba, 2012, Nairobi,
tulipokea taarifa ya hatua iliyofikiwa kuhusu mchakato wa kutaka
kuanzishwa kwa Shirikisho. Mkutano huo uliagiza nchi wanachama
kujadiliana zaidi kuhusu mpango kazi wa kufikia Shirikisho la Kisiasa na
mpango wa kutekeleza mapendekezo mengine yaliyotolewa na Timu ya
Wataalamu. Inategemewa kuwa Baraza la Mawaziri litawasilisha
mapendekezo ya majadiliano hayo katika Mkutano wa 15 wa Wakuu wa Nchi
mwezi Novemba, 2013. Iweje leo wenzetu hawa waamue kuanzisha mchakato
wao wa kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika;
Kwa kweli huwa najiuliza maswali mengi na kukosa majibu kuhusu
nini kinachoendelea kufanywa na viongozi wenzangu watatu na kwa nini!
Nakosa majibu ya uhakika. Je wenzetu wamekosa imani na Jumuiya ya
Afrika Mashariki na je wanataka kuunda yao? Je wanaichukia nchi yetu na
hivyo wameamua kutufanyia vitimbi tutoke! Au sijui wanachuki na mimi!
Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kuwa hatuna mpango wa kutoka
(kama vijana wasemavyo hatoki mtu hapa). Tupo na tutaendelea kuwepo!
Mheshimiwa Spika;
Tanzania haijafanya jambo lo lote baya dhidi ya Jumuiya
au nchi yo yote mwanachama. Na ukweli ni kwamba ni mwanachama
mvumilivu, mtiifu na mwaminifu kwa Jumuiya. Tunatimiza ipasavyo wajibu
wetu kwa Jumuiya na kushiriki kwa ukamilifu katika ujenzi wake na
utengamano ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Sabahu ya wenzetu
watatu kuamua kufanya mambo yahusuyo Jumuiya yetu peke yao kwa kweli
haieleweki.
Mheshimiwa Spika;
Tunasikia eti kuwa baadhi yao walipoulizwa kwa nini wengine hatupo
wakasema kuwa wao wametangulia na sisi tutakapokuwa tayari tutajiunga.
Yaani wana Umoja wa Waliokuwa Tayari (Coalition of the Willing). Hivi
ni nani hayuko tayari (who is not willing?) Haiwezekani watu waitane
wenyewe bila ya kutualika halafu wadai kuwa wao ndiyo wako tayari na
kujenga dhana kuwa sisi wasiotualika ndiyo ambao hatuko tayari. Madai
hayo hayana ukweli. Ni vyema waseme ukweli. Kama walitualika tukakataa
ndiyo wanaweza kusema hayo.
Mheshimiwa Spika;
Kumekuwepo na madai kutoka kwa baadhi ya wenzetu, eti kwamba
Tanzania haina moyo wala dhamira ya dhati ya kuendeleza utengamano wa
Afrika Mashariki. Kwa sababu hiyo inasemekana eti nchi yetu imekuwa
kikwazo kwa maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba Tanzania
tunawachelewesha wengine kupiga hatua za haraka. Wanadai kama siyo
hivyo Jumuiya ya Afrika Mashariki ingekuwa mbali kwa maendeleo. Maneno
hayo yamekuwa yanarudiwa au kujirudia mara nyingi kiasi cha kuwafanya
baadhi ya watu wa Afrika Mashariki na hata kwingineko duniani waamini
hivyo.
Mheshimiwa Spika;
Napenda kusema kwa dhati ya moyo wangu kwamba madai hayo hayana
ukweli wo wote. Isitoshe hata sababu zinazotolewa kuthibitisha ukweli
wake hazina mashiko. Hazifanani na ukweli kuhusu Tanzania na Watanzania
walivyo. Tanzania ni muumini wa dhati wa umoja na utengamano wa nchi
za Afrika Mashariki na Afrika. Tumethibitisha hivyo kwa vitendo kwa
kuunganisha nchi zetu mbili huru yaani Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na
Jamhuri ya Tanganyika na kuwa taifa moja liitwalo Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Muungano wa nchi zetu mbili ndio pekee uliodumu kwa muda
mrefu kuliko yote Afrika.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania ni mwanachama mwaminifu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
kwa maana ya kutekeleza Mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo, kwa Itifaki
zake na maamuzi halali ya vikao na taasisi za Jumuiya. Kama lipo jambo
ambalo hatujalifanya ilivyotakiwa itakuwa ni kwa sababu za msingi na
siyo kwa sababu ya kupuuza Jumuiya. Tunaithamini sana Jumuiya na tumeipa
kipaumbele cha juu. Hatuwezi kuhangaika kwa gharama kubwa ya muda
wetu, fedha zetu na kutoa mchango wa hali na mali kuianzisha, kujenga na
kuifikisha Jumuiya hapa ilipo halafu tuwe ni watu tunaoongoza
kutokuipenda na kudhoofisha maendeleo na ustawi wake. Ni maneno ya
kushangaza na wala hayaingii akilini. Ama kweli akutukanae hakuchagulii
tusi.
Mheshimiwa Spika;
Nionavyo mimi msimamo wetu kuhusu kuharakisha Shirikisho
na masuala ya ardhi, ajira, uhamiaji, pengine ndiyo yanayotuletea hisia
zisizokuwa sahihi juu yetu. Mimi siamini kama kuna mengine. Hata
hivyo, napata taabu kuamini kwamba kutofautiana kwa mawazo katika mambo
hayo kutapelekea baadhi ya wenzetu wasipende hata kushirikiana nasi kwa
mambo ambayo hayana matatizo na tumekuwa tunashirikiana vizuri.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania imekuwa inawasihi wanachama wenzetu kuwa tujenge Jumuiya
yetu hatua moja baada ya nyingine kama ilivyo kwenye Mkataba ulioanzisha
Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hatuna tatizo la kuongeza kasi ya ujenzi
wa Jumuiya lakini tusivuke hatua yo yote. Tusiende kasi ya kupindukia.
Mkataba unaelekeza tunaanza na Umoja wa Forodha, inafuatia Soko la
Pamoja kisha Umoja wa Kifedha na hatimaye Shirikisho la Kisiasa.
Mheshimiwa Spika;
Ni kweli kabisa hatukuunga mkono
kuharakisha Shirikisho la Kisasa kabla ya kukamilisha baadhi ya hatua.
Na, tulifanya hivyo kwa nia njema ya kutaka Shirikisho lijengwe juu ya
msingi imara. Na, msingi huo si mwingine bali utengamano wa kiuchumi
kwa maana ya Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja na Umoja wa Kifedha
zilizojengeka vizuri na kufanya kazi ipasavyo na kunufaisha wanachama
wote sawia.
Mheshimiwa Spika;
Lazima tutambue ukweli kuwa kunufaika kiuchumi ndicho
kichocheo kikubwa cha nchi kujiunga na kuendelea kuwa mwanachama wa
Jumuiya yetu. Kama mambo ya kiuchumi yakipangika vizuri na kila nchi
ikanufaika sawia, unajenga msingi imara kwa Shirikisho la Kisiasa
kustawi na kudumu. Kama ngazi hizi tatu za awali hazitashughulikiwa
vizuri na nchi wanachama zikahisi hazinufaiki ipasavyo, Shirikisho
litayumba au kuyumbishwa hivyo kudumu kwake kutakuwa kwa mashaka.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania ni kati ya zile nchi zinazotaka ngazi zote za
mchakato wa utengamano zitekelezwe moja baada ya nyingine bila kuruka
hata moja. Kwa msimamo na mtazamo wetu, Shirikisho iwe ndiyo hatua ya
mwisho. Na huo siyo msimamo wangu au wa Serikali peke yake, ndiyo
msimamo wa Watanzania walio wengi.
Bila ya shaka sote tutakumbuka kuwa mwaka 2006 Wakuu wa
Nchi Wanachama wa Jumuiya waliunda Kamati Maalum katika kila nchi
kukusanya maoni ya wananchi kuhusu kuharakisha Shirikisho la Afrika
Mashariki. Kwa hapa nchini Kamati hiyo iliongozwa na Profesa Samwel
Wangwe na katika taarifa yake, Kamati ilieleza kuwaasilimia 74.4 ya Watanzania wanaunga mkono kuwepo kwa Shirikisho lakini ni asilimia 25.4 tu ndiyo waliunga mkono kuharakishwa kwake.
Mheshimiwa Spika;
Takwimu hizi zinaelezea ukweli kuhusu hisia za
Watanzania, kuhusu kuwepo kwa Shirikisho na kasi ya utekelezaji wake.
Watanzania wengi sana wanaunga mkono kuwepo kwa Shirikisho la Afrika
Mashariki lakini wanataka jambo hilo lisifanywe haraka haraka. Wanataka
lifanywe kwa umakini mkubwa na tuende hatua kwa hatua kama
ilivyoainishwa katika Mkataba uliounda Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika;
Sera na msimamo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania inakwenda sambamba na ile ya wananchi wa Tanzania. Ndiyo maana
tumeafiki mapendekezo ya Kamati ile ya mwaka 2004iliyoongozwa na
Mheshimiwa Amos Wako wakati ule akiwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya.
Kamati hiyo iliundwa kupendekeza namna ya kuharakisha utekelezaji wa
mchakato wa utengamano wa Afrika Mashariki.
Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umetamka muda wa
kutekeleza ngazi ya Umoja wa Forodha lakini uko kimya kuhusu ngazi
zilizofuata. Ili kuondoa kasoro hiyo na kwa nia ya kuharakisha
Shirikisho Kamati ilipewa jukumu la kutoa maoni na mapendekezo juu ya
namna ya kufanya hivyo. Kamati ilifanya kazi nzuri ya kupata maoni na
hisia za watu wa makundi mbalimbali katika nchi wanachama kuhusu ujenzi
wa Jumuiya na utengamano.
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa Tanzania kwa mfano, Kamati ya Mheshimiwa
Amos Wako ilitambua hisia za Watanzania kuhusu ardhi na ajira na
kupendekezwa kuwa masuala hayo yabaki kwenye mamlaka ya nchi wanachama
kuamua. Kuhusu mchakato wa utengamano Kamati ilipendekeza kwanza kwamba
mchakato wa ujenzi wa Umoja wa Forodha uachwe mpaka ufike ukomo wake wa
miaka mitano. Baada ya hapo muda wa kutekelezwa ngazi zinazofuata
unaweza kupunguzwa. Kwa mfano walipendekeza kuwa matayarisho ya kuunda
Soko la Pamoja yaanze hata kabla ya mchakato wa Umoja wa Forodha kufika
mwisho ili mara wakati huo ukifikiwa Soko la Pamoja linaanze. Hivyo
hivyo mara baada ya ngazi hiyo kuanza matayarisho ya kuanza ngazi ya
Umoja wa Kifedha yanaanza. Ngazi hiyo nayo ikianza matayarisho ya
kuunda Shirikisho yanaanza. Kamati pia imetoa mapendekezo ya namna ya
kufikia uamuzi kuhusu Shirikisho kwamba wananchi wa nchi wanachama
wataamua kwa kura. Tukifuata mapendekezo ya Kamati ya Mheshimiwa Amos
Wako na wenzake kama tufanyavyo sasa Tanzania haina matatizo nayo.
Mheshimiwa Spika;
Baada ya kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na wana-Afrika
Mashariki kuhusu ujenzi wa Jumuiya yao inasikitisha kuona vinafanyika
vitendo vinavyoanzisha mivutano kuhusu mambo yaliyokwisha fanyiwa kazi
na kuamuliwa. Tunapata taabu zaidi pale watu wanapobagua wenzao na
wanapofanya mambo yanayopingana na Mkataba wa Jumuiya na Itifaki zake.
Kwa kweli kama mwenendo huu hautabadilika sijui mambo yatakuwaje mbele
ya safari.
Mheshimiwa Spika;
Nchi yetu inapenda kuona kuwa tunakuwa na Jumuiya ya Afrika
Mashariki iliyo imara na iliyo endelevu. Jumuiya ambayo inaendeshwa
vizuri, mambo yake ni mazuri na nchi zote wanachama na watu wake
wananufaika nayo, na hivyo wanaifurahia. Tanzania haina tatizo na
kuharakisha mchakato wa utengamano, lakini tunapata taabu kuruka baadhi
ya hatua kabla hazijakamilika. Tunawaomba wenzetu kuwa makini katika
kila hatua tunayochukua. Bila ya kufanya hivyo, Jumuiya yetu itakuwa
imejengeka katika msingi dhaifu hivyo ustawi na uhai wake utakuwa na
changamoto nyingi. Hatupendi ya mwaka 1977 yatokee tena.
Mheshimiwa Spika;
Napenda kuwahakikishia kuwa Tanzania
itaendelea kushiriki katika shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki na
kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki kwa kuzingatia matakwa ya
Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Itifaki zake. Tutafanya kila
tuwezalo kuhakikisha kuwa Jumuiya haidhoofiki wala kufa. Na iwapo
itadhoofika au kufa kamwe hatutaki Tanzania inyooshewe kidole kuwa
chanzo wala kichocheo chake. Ndiyo maana, hatutachoka kuzungumza na
wenzetu kuhakikisha kuwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki inaendelea
kustawi.
Tutaendelea kukumbushana umuhimu wa kufanya mambo yanayojenga na
kuepuka yale yanayoweza kubomoa.
Tutakumbushana umuhimu wa kuheshimu
matakwa na masharti ya Mkataba ulioanzisha Jumuiya, Itifaki zake na
maamuzi halali ya vikao rasmi na asasi za Jumuiya. Tukifanya hivyo
Jumuiya ya Afrika ya Mashariki itadumu, itazidi kustawi na kunufaisha
nchi wanachama na watu wake kama yalivyo malengo na madhumuni ya kuundwa
kwake.
Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania
Idumu Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mheshimiwa Spika na
Waheshimiwa Wabunge;
Asanteni sana kwa kunisikiliza