tangazo
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linamshikilia John Mayunga (56) mkazi wa Kiwalani kwa tuhuma za kumjeruhi kwa mapanga sehemu za kichwani na usoni, Dk. Sengondo Mvungi.
Taarifa hizo zimetolewa ikiwa ni siku moja tangu mwanasheria huyo
maarufu kufariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya
Millpark nchini Afrika Kusini juzi alasiri.
Dk. Mvungi alivamiwa Novemba 3, mwaka huu, saa 6:30 usiku na watu
wanaosadikiwa kuwa majambazi, nyumbani kwake Kibamba, Kata ya Mpiji
Magohe, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam kisha kujeruhiwa na kuporwa
sialaha, kompyuta na fedha.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamishna wa kanda hiyo,
Suleiman Kova, alisema askari walipata taarifa kutoka kwa raia wema
kwamba Mayunga alishiriki kikamilifu na wenzake katika tukio hilo.
Alisema kuwa waliambiwa kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa maeneo ya Mtaa wa
Twiga Jangwani akiangalia televisheni, ndipo akakamatwa na kuhojiwa
ambapo alikubali kuhusika moja kwa moja na tukio hilo.
Kova alisema taratibu za upekuzi zilifanyika na katika harakati hizo
kwenye chumba anacholala, ilipatikana silaha ambayo ni bastola aina ya
Revolver namba BDN 6111 pamoja na risasi 21 za bunduki hiyo.
Vitu vingine vilivyokutwa ni vifaa vya mlipuko/baruti aina ya
explogel yenye muundo wa sausage, tambi 2 ambazo ni viwashio vya baruti
(detonator) na milipuko 4 ambayo imeunganishwa na tambi tayari kwa
kutumia.
“Mtuhumiwa Mayunga alipohojiwa kuhusu umiliki wa silaha hiyo hakuwa
na kibali chochote cha umiliki, badala yake alieleza ni kati ya vitu
walivyoiba yeye na wenzake nyumbani kwa Dk. Mvungi,” alisema.
Alisema kuwa silaha hiyo ilitambuliwa na familia ya marehemu na
kwamba ilikuwa chini ya himaya yake. Kwamba kumbukumbu za maandishi
zinaonyesha kuwa ni jambazi mzoefu na hivi karibuni alimaliza kifungo
cha miaka saba jela kwa makosa ya ujambazi.