Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Said Mwema.( PICHA ya MAKTABA)
*****
Watu watatu, akiwamo askari polisi wamefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa baada ya kuzuka mapambano kati ya polisi na raia katika Kijiji cha Igwati, Tarafa ya Malinyi Wilaya ya Ulanga, Morogoro.

Diwani wa Kata ya Malinyi, Said Kila aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Leon Chikwita, Andrew Likomoka na Edson Kidunda.
Alisema mmoja wa majeruhi Idelfonce Malenga (35),
hali yake ni mbaya baada ya kupigwa risasi shavuni. Majeruhi wawili
majina yao hayakufahamika mara moja.
Diwani Kila alisema mauaji hayo yalitokea baada ya
kundi la wakulima kuvamia Kituo cha Polisi Malinyi kushinikiza kuachiwa
kwa wenzao watatu waliokuwa wanashikiliwa kwa tuhuma za kumuua mfugaji
mmoja wa kijiji hicho hivi karibuni.
“Baada ya kupata taarifa za kukamatwa kwa wenzao
walifika kituo cha polisi ambako, hawakuwakuta watuhumiwa hao kwani
walikuwa wamehamishiwa kituo kingine,” alisema diwani huyo.
Alisema katika jitihada za kulinda kituo, polisi
walitoa tahadhari mbalimbali za kuwataka wananchi hao kutawanyika
ikiwamo kupiga mabomu ya machozi, lakini waliendelea kukaidi amri hiyo
na badala yake walizidi kujikusanya na kukivamia na kisha kukichoma moto
pamoja na gari la askari lililokuwapo. Katika shambulizi hilo, ndipo
mauaji hayo yalipotokea.
Chagonja eneo la tukio
Kutokana na tukio hilo, Mkuu wa Jeshi la Polisi,
IGP Said Mwema ametuma timu maalumu ikiongozwa na Kamishna wa Operesheni
na Mafunzo, Paul Chagonja kwenda kuongeza nguvu katika operesheni ya
kuwasaka na kuwakamata wote waliohusika na tukio hilo.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso ilisema
jana katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa, IGP Mwema ametoa
wito kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro hususan, Kata ya Malinyi kuwa
watulivu na kuendelea kutoa ushirikiano kwa Polisi wakati uchunguzi
ukiendelea.
Chanzo cha mgogoro
Mgogoro kati ya wafugaji na wakulima wa Igwati
ulianza Desemba 13, mwaka huu wakati kundi la wananchi lilipomkamata
mfugaji huyo na kumpeleka katika ofisi za kijiji.
Ilidaiwa kuwa baada ya kumfikisha, mtendaji wa
kijiji alimfungia mtuhumiwa huyo ofisini kwake na kuanza kuhoji sababu
za wananchi kumkamata jambo ambalo linaelezwa kwamba liliwakera na
kuanza kumshambulia hadi kuikimbia ofisi na kumwacha mfugaji huyo ambaye
alishambuliwa na kuuawa.
Kitendo cha kukamatwa na kupigwa hadi kuuawa kwa mfugaji huyo kinadaiwa kuwa kilikuwa cha kulipiza kisasi baada ya wafugaji kuvamia nyumbani kwa Mjumbe wa Kamati ya Mazingira, Victoria Marietha na kumjeruhi vibaya kisha kufariki dunia katika Hospitali ya Lugala, Malinyi alikokuwa akipatiwa matibabu.
-Mwananchi.

tangazo