tangazo
Wakati Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya akiahidi kuwasaka na kuwakamata walioua watu katika eneo la Westgate, Nairobi, Serikali ya Tanzania inawasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo ili kufahamu kama raia wake walikuwa miongoni mwa watu walioathiriwa na shambulio hilo.
Watu 69 waliuawa na 107 kujeruhiwa wakati magaidi walipovamia juzi kwenye eneo la maduka jijini Nairobi.
Bado askari wa Kenya wakisaidiwa na maofisa wa
Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) na wale wa Shirika la Ujasusi la
Israel (Mossad) wanapambana na magaidi hao.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje,
John Haule alisema jana kuwa Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk Batilda
Buriani alikutana na maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya lakini
hadi jana hakukuwa na taarifa zozote za Watanzania kuwepo kwenye tukio
hilo.
“Tunaendelea kuwasiliana na ubalozi wetu Nairobi
kujua hali ilivyo, lakini hadi sasa hatuna taarifa rasmi kuhusiana na
raia wetu kuwepo kwenye tukio hilo. Nimezungumza na balozi wetu
ameniambia bado anaendelea kukutana na wenzetu wa Mambo ya Nje wa
Kenya,” alisema Haule.
Akihutubia taifa kwenye Ikulu ya Kenya jana, Rais
Kenyatta alisema Serikali yake haitarudi nyuma katika kupambana na
ugaidi mahali popote, huku akisema ugaidi si tatizo la Kenya pekee, bali
la kimataifa na kwamba litamalizwa kwa nchi kushirikiana.
“Tunatakiwa kuwa kitu kimoja na mpaka sasa Idara
ya Usalama inaendelea kuimarisha ulinzi eneo husika, magaidi waliopo
katika jengo ni kati ya 10 hadi 15. Tutashinda vita hii ya ugaidi kwa
umoja wetu na tuweke tofauti zetu pembeni,” alisema.
Awali, Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila
Odinga aliwataka Wakenya kutokuifananisha vita ya ugaidi na udini wala
ukabila na kusisitiza kuwa matukio kama hayo yametokea hata katika nchi
za Ulaya.
“Mataifa ya kigeni yasisitishe safari za kutoka ndani na nje ya Kenya, tusigawanyike kwa njia yoyote ile,” alisema Odinga.